UNAICHUKULIAJE Valentine’s day?
Huwa una ratiba ya kufanya nini kila mwaka kwa ajili ya siku hiyo? Rafiki zangu, inawezekana mnadhani bado mbali sana na pengine mnanishangaa kuanza kuandika mada ya valentine mapema kiasi hiki!Zimebaki siku kumi tu kuifikia siku hiyo, ndiyo maana nikaona hapa katika Let’s Talk About Love, ukurasa maalumu kwa ajili ya kuzungumzia mambo ya mapenzi, nielezee hili japo kwa dodoso.
Nimeanza na maswali na pengine niendelee kuuliza, kabla ya kuzama moja kwa moja kwenye mada husika. Unadhani unatakiwa kufanya nini ili kuifanya siku hiyo kuwa nzuri kwako? Yapo mambo mengi sana ya kufanya, lakini kabla ya kuingia huko tuone kwanza maana yake, japo kwa kifupi sana.
VALENTINE’S DAY
Valentine ni neno la Kiingereza, lenye maana ya upendo – kupendana – wapendanao. Kwa Kiswahili rahisi tunaiita siku hiyo Sikukuu ya Wapendanao. Asili hasa ya siku hiyo ni huko Roma.Inaelezwa kwamba, siku hiyo huadhimishwa kama kumbukumbu ya Padre Valentino ambaye aliuawa na Utawala wa Kirumi uliokuwa chini ya Mfalme Claudia kwa kosa la kutetea waumini wake wafunge ndoa.
Ilivyo ni kwamba, Mtakatifu Valentino alikerwa na Utawala wa Kirumi ambao uliwakataza vijana kufunga ndoa na badala yake kwenda vitani. Kwa msingi huo vijana wakawa na vimada nje hivyo kwenda kinyume na utaribu na maagizo ya imani aliyoisimamia Mtakatifu Valentino.
Kwa sababu hakupenda hilo liendelee, akaamua kuendesha zoezi la kuwafungisha ndoa vijana kwenye makatakabo (mahandaki chini ya kanisa) kwa siri kubwa.Hata hivyo, aligunduliwa na kufungwa na baadaye kuhukumiwa kifo.Kwa msingu huo, kwa sababu Mtakatifu Valentino aliauwa siku na tarehe kama hiyo, ikatangazwa rasmi kuandhishwa kwa ajili ya kumkumbuka kama Baba wa Upendo – mtetezi wa wanandoa.
Awali ilianza kuadhimishwa huko Roma, lakini baadaye ikaenea katika nchi za Magharibi na dunia nzima kwa ujumla. Wakati mapokeo ya kuadhimisha siku hii yalipoanza, ilionekana kama ni ya kidini zaidi, lakini baadaye ilipochunguzwa mantiki ya uadhimishaji wenyewe, ikaonekana kuwa na maana kwa watu wa madhehebu yote.Aliyetangaza rasmi kuadhimisha siku hiyo ni Papa Gelasius, ambapo alisema ikumbukwe kama ishara ya kumuenzi mtetezi wa ndoa Mtakatifu Valentino.
SI VURUGU/NGONO/UCHAFU
Baadhi ya watu wameibadilisha maana ya siku hii muhimu kwa wapendanao. Wenyewe wanahisi kuwa ni siku ya kufanya mambo yasiyofaa. Kwao, wapendanao ni ngono. Kuna ambao huanzisha uhusiano siku hiyo kwa lengo la kupata mtu wa kustarehe naye, hili ni kosa.Kuna baadhi wamekuwa wakifanya vurugu na kila aina ya uchafu. Si maana yake. Kama nilivyotangulia kusema, ni siku ya kuoneshana namna mnavyopendana na kuthaminiana. Msingi hasa hapa ni pendo la kweli.
UNAADHIMISHAJE?
Nilianza mada yangu kwa kuuliza maswali, sasa ni wakati wa kuyapatia majibu. Wewe unaadhimishaje siku hiyo? Huwa una kawaida ya kufanya nini kwa ajili ya siku hiyo muhimu kwa ajili ya penzi lako?
Tunatofautiana kufikiria, kupanga na kufanya mambo. Inawezekana umezoea kumchukua mpenzi wako na kwenda naye katika hoteli ya kitalii kisha mnakula raha zenu huko halafu sikukuu inakuwa imeisha!
Si vibaya! Labda una mpango wa kushinda na mwenzako ndani siku nzima. Mwingine inawezekana anapanga kwenda katika ukumbi wa burudani na kusikiliza nyimbo nzuri za wapendanao. Si mawazo mabaya.
Hata hivyo, rafiki zangu lazima ufikirie kufanya jambo kubwa, maalumu ambalo si tu halitasahaulika bali litatengeneza kitu kikubwa katika historia ya mapenzi yenu.Inawezekana umeumiza kichwa sana ukijaribu kufikiria kitu cha kufanya kwa ajili ya kunogesha penzi lako, kuifanya ndoa yako kuwa imara, lakini uwezo wako wa kufikiri umefika mwisho na hujapata cha kufanya.
Vipi, umewahi kufikiria kuhusu kufanya hafla ya wapendanao? Yes! Hafla ya wapendanao ni nzuri, maana huwakutanisha wenzi na kupanga pamoja namna ya kuifanya siku hiyo kuwa yenye kuvutia na kujadiliana kwa pamoja namna ya kuishi na wenzi wenu.Hapa nimekuandalia vipenegele vichache, vitakavyokuongoza namna ya kuandaa hafla hiyo. Karibu tujifunze rafiki yangu mpenzi.
KWA NINI UANDAE HAFLA?
Kuna mengi, lakini kubwa zaidi ni kumfanya mwezi wako ajione wa pekee kwa kuandaa sherehe kwa ajili ya siku hiyo muhimu. Ukiachana na hilo, pia utakuwa umeonesha upendo wako kwa wengine, kwa kuwaunganisha sehemu moja. Humuongezea kujiamini na kuunganisha urafiki, maana ni lazima waalikwe watu wengine ambao watakuwa wawili wawili (couple).
ANDAA KICHWANI MWAKO
Hafla hii inakuwa na utamu zaidi kama utamshtukiza (surprise) mpenzi wako. Inakuwa na ubora zaidi akiwa hajui kama una mpango wa kuandaa sherehe.Bila shaka siku ya wapendanao, lazima utakuwa naye, ni siku hiyo ambayo utamwambia, tena ikiwezekana saa chache kabla au atafahamu akiwa tayari eneo la tukio.