HEALTHY

JUISI NA FAIDA ZAKE MWILINI


LEO nitaongelea faida za kunywa juisi katika mwili wa binadamu.
Kuna juisi za aina mbalimbali na matumizi yake yanategemea na malengo ya mtumiaji. Inawezekana watumiaji wengi wanakunywa juisi bila kujua umuhimu au kazi yake mwilini.
Safu hii itaeleza utumie juisi gani na wakati gani na nitaeleza pia jinsi ya kutengeneza na kazi zake.

JUISI YA TIKITI MAJI
Chukua tikiti maji (Watermelon), osha kisha likate vipande na chukua nyama yake ya ndani ambayo utaisaga na kupata juisi.

Faida yake
Juisi hii ina uwezo wa kusafisha figo pamoja na njia ya mkojo yaani Urethra. Inazuia unene (Obesity) kwa kuwa na kiwango kidogo cha calories.

JUISI YA KAROTI NA APPLE 
Hutengenezwa kwa kusaga matunda hayo na kukamua maji yake na maelekezo yake yapo hapo chini.

JINSI YA KUTENGENEZA
Chukua kiasi cha karoti na apple kinachotosha kutengeneza juisi kwa kiasi ulichokusudia. Anza kuandaa juisi yako kwa kuosha na kumenya karoti na apple kisha katakata katika vipande vidogo vinavyoweza kusagika kirahisi kwenye blenda. Saga mchanganyiko wako ili upate juisi. Baada ya kupata mchanganyiko wa juisi yako unaweza kuongeza asali japokuwa siyo lazima kwa kuwa matunda hayo yana sukari.

Faida yake
Juisi hii ina uwezo wa kutunza ngozi yako kwani tunda la apple linaondoa uchafu kwenye ngozi na karoti nayo kwa kutumia kirutubisho cha beta-karotini chenye uwezo wa kutengeneza vitamini A huweza kulinda na kurejesha uhai katika ngozi ambapo inaifanya ionekane nyororo.
Pia juisi hii huweza kulifanya tumbo lako kuwa safi kwani husafisha tumbo na kuondoa uchafu tumboni. Aidha, juisi hii inafanya ini lifanye kazi yake vizuri kwa kulainisha nyongo na kusaidia kuondoa uchafu.

JUISI YA VIAZI MVIRINGO
Chukua viazi mviringo vinavyotosha kwa juisi. Andaa kwa kuviosha na kumenya kisha katakata vipande vidogo kwa ajili ya kuvisaga. Saga ili upate juisi uliyoikusudia.
Faida yakeJuisi hii inatumika kama dawa ya kuondoa au kupunguza asidi au gesi tumboni. Juisi ya viazi mviringo inaweza kusaidia kupunguza matatizo ya figo, kisukari, unene au kitambi.

JUISI YA MBOGAMBOGA

Juisi hii ina mchanganyiko wa mbogamboga ambazo mtumiaji hupenda kama vile matango, karoti na nyanya. Maandalizi yake ni kama juisi nyingine.
Anza kwa kuosha mbogamboga hizo kisha menya na kukatakata vipande. Saga mchanganyiko huo kwenye blenda ili upate juisi uliyoikusudia.

Faida yake
Juisi hii inasaidia kuzuia kansa hasa ile ya kwenye mfumo wa kumeng`enya chakula, kukinga mapafu na mishipa ya artery. Pia inasaidia kuimarisha kinga.
Kwa aina hizo chache za juisi unaweza kujua umuhimu wa juisi za matunda na mbogamboga tunazotumia. Kwa leo ninaishia hapo, siku zijazo nitaendelea kukupatia ufahamu kwa aina zingine za juisi pamoja na kazi zake.



 NANASI: KINGA DHIDI YA MAGONJWA YA UVIMBE


MWILI unapokosa kinga imara, huwa katika hatari ya kushambuliwa na kila aina ya magonjwa. Katika orodha hiyo ya magonjwa, yamo pia yale ya kutokwa uvimbe, yakiwemo majipu, kitaalamu yanajulikana kama ‘Inflamatory deseases’!.
Katika kukabiliana na matatizo kama hayo, nanasi ni moja kati ya matunda yenye vitamini nyingi na virutubisho vingine vyenye uwezo wa kutoa kinga kwenye mwili wako dhidi ya magonjwa hayo na mengine.
Siri na umuhimu wa nanasi, upo kwenye kirutubisho aina ya ‘Bromelain’ ambacho kinapatikana kwa wingi kwenye tunda hili na hivyo kulifanya kuwa tunda muhimu sana katika kujenga na kuimarisha kinga ya mwili.
Ukilipa umuhimu na ukiliweka nanasi katika orodha ya matunda unayokula mara kwa mara, utajiepusha na utajipa kinga dhidi ya magonjwa mengi, hususan ugonjwa wa kuwashwa na kuvimba koo, ugonjwa wa Baridi Yabisi (Arthritis) na ugonjwa gauti (Gout).
Ili upate kinga dhindi ya maradhi hayo kwa kula nanasi, unashauriwa kula nanasi kabla au baada ya kula mlo wako, usile nanasi pamoja na chakula kingine kwa wakati mmoja, kwa kufanya hivyo, virutubisho vitafanyakazi nyingine tofauti na uliyokusudia. Faida nyingine za nanasi ni kama ifuatvyo;

USAGAJI WA CHAKULA

Nanasi lina virutubisho vinavyouwezesha mfumo wa usagaji chakula tumboni kufanya kazi yake ipasavyo, pindi mfumo huu unapowezeshwa kufanyakazi yake vizuri, mtu huweza kupata choo laini na kwa wakati kama inavyotakiwa.

KINGA YA MWILI
Nanasi linaaminika pia kuwa miongoni mwa matunda yenye chanzo kizuri cha vitamin C ambayo kazi yake ni kuupa mwili kinga dhidi ya ‘wavamizi’ mbalimbali (free radicals), ambao wanapoingia mwilini, kazi yao hua ni kuharibu chembembe hai za mwili.
Kwa kuongezea, vitamini C inaaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili, hivyo kuifanya kuwa kinga ya magonjwa madogo kama vile mafua, kikohozi, homa na maambukizi mengine. 
 
CHANZO CHA MADINI
Mbali ya kuwa ni chanzo kizuri cha vitamin C, nanasi pia ni chanzo kizuri cha madini aina ya ‘manganese’ ambayo yanaaminika kuwa na uwezo wa kuboresha ufanisi wa vimeng’enyo mbalimbali vya mwili, vikiwemo vya kuzalisha nishati na kinga ya mwili. Halikadhalika tunda hili lina kiwango cha kutosha cha vitamin B1 (thiamin).

KUIMARISHA NURU YA MACHO
Inawezekana karoti ikawa ndiyo inayojulikana na watu wengi kuwa na uwezo wa kuimarisha nuru ya macho, lakini nanasi nalo lina uwezo mkubwa wa kuimarisha nuru ya macho. Utafiti unaonesha kuwa ulaji wa tunda hili na matunda mengine, kiasi cha milo mitatu kwa siku, kunaondoa hatari ya kupungua kwa nuru ya macho kwa asilimia 36 kwa watu wazima.

NANASI LILILO BORA

Nanasi lililo bora ni lile kubwa na lililoiva vizuri. Wakati ni kweli kwamba nanasi kubwa lina nyama nyingi kuliko nanasi dogo, lakini hakuna tofauti ya ubora wa virutubisho kati ya nanasi dogo na kubwa, ilimradi lisiwe limeoza au lenye michubuko mingi. Hivyo chagua nanasi lililoiva vizuri na lenye kunukia.
Mara baada ya nanasi kumenywa na kukatwa vipande, linatakiwa kuliwa mara moja, iwapo litahifadhiwa kwenye jokofu kwa ajili ya kuliwa baadaye, njia sahihi ya kuhifadhi ni kuliweka kwenye chombo chenye mfuniko (container) ili kuhifadhi virutubisho vyake kwa kipindi hadi cha siku tano bila kupoteza ubora wake, ikiwa pamoja na ladha. Unaweza kula vipande vya nanasi au juisi yake, kote kuna faida.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...