Dec 13, 2011

Simu, mitandao ya kijamii, vinawatesa wengi

si kwa mtu mmoja au wawili, bila shaka utakuwa umeshashuhudia wapenzi wakitengana, wanandoa wakikosa suluhu kwa sababu ya SMS au simu. Baadhi wapo katika uhusiano wa ‘ilimradi siku zinaenda’, yaani ni mashaka tupu.

Kama si upande huo wa shilingi, basi utakuwa umeshajionea jinsi watu wanavyokosa amani mbele ya wapenzi wao. Wakizima simu muda wote au wakiishia kuwapiga marufuku wasiziguse kwa kuhofia siri zao kugundulika.

Unadhani hayo ndiyo mapenzi? La hasha! Wawili wanaopendana, ni sharti kati yao kuwe na amani, upendo, uaminifu na uhuru wa kila mmoja kwa mwenzake. Wanaowekeana mipaka, hao wamepata alama ‘F’ katika taaluma ya ‘malavidavi’.

Inawezekana hata upande huo ukawa ni mgeni kwako, lakini huu utakuwa unaujua. Ipo Kasumba ya baadhi ya watu kutunza namba za simu za wapenzi wao wa pembeni kwa majina tofauti.

Wanawake ‘kusevu’ majina ya kike, wakati wanaume wakiwaandika wenzi wao wa nje kama wanaume wenzao. Husna kuitwa Hussein, Nasra kuandikwa Nassor au Jane kama John.

Wanawake nao, Joseph kuandika Josephine, Justin kuita Justina au kumuandika Ramadhan kama Swaumu. Umenipata? Hayo ndiyo mapenzi ya kileo na balaa lililopo katika simu za mkononi.

Dunia inavyopanuka ndivyo mambo ya utandawazi yanavyoshamiri. Simu za mkononi zilitikisa lakini kwa sasa Facebook inatajwa kwa sana. Kuna watu sasa hivi wanaishi roho juu kila wakijua wapenzi wao wapo ‘online’. Kuna jamii inaanzisha uhusiano mpya kila siku.

Nikiwa online katika ukurasa wangu wiki iliyopita, kuna ndugu mmoja aliniuliza: “Luqman, hujaona jinsi Facebook inavyohamisha mapenzi. Watu wanaanzisha uhusiano mpya kila siku mtandaoni. Hali ilivyo, Facebook inapunguza kiwango cha uaminifu.”

Ni hoja inayohitaji uchambuzi wa kina. Ipo wazi kwamba Facebook inagusa mitima ya idadi kubwa ya watu. Na sipingani na mtazamo wa rafiki yangu kuwa kuna watu wanashinda mitandaoni kuwinda wapenzi badala ya kukuza mtandao wa maisha, biashara na kadhalika.

Kuna vijana wanatumia muda wao mtandaoni kusaka wanawake wakubwa ili walelewe. Lipo kundi la ‘wadada’ wanaohangaikia mabwana wa nje hususan Wazungu. Mtu ana mpenzi wake lakini anaanzisha urafiki na baadaye mapenzi baada ya ‘kuchati’ naye mara kadhaa. Maendeleo yamekuja na mambo leo!

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...